Jenga tabia ya kumshukuru Mungu kwa kila jambo katika maisha yako, liwe baya au jema. Wakati mwingine kuna mambo unakutana nayo kwa ajili ya kukukomaza, kukufunza au kukuweka karibu na Mungu. Yamkini umesikia, umejionea au umepatwa na jambo hili.
Huo ndiyo ukweli kuwa, ukimsomesha mpenzi wako, aidha, ni wa kiume au kike kwa kutegemea aje awe mkeo au mumeo, basi tegemea mambo mawili;
KUFIKIA MALENGO
Kama kweli mwanamke au mwanaume ambaye umemsaidia kwa kumsomesha ana mapenzi ya dhati, inawezekana kabisa mkafikia malengo yenu ya kuwa mke na mume. Ingawa hili huwa linafikiwa kwa kiwango kidogo mno kwani inawezekana kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu pekee ambaye atakuwa amepanga ninyi muungane iwe kwa mapito ya aina yeyote ile, lakini mwisho wa siku lazima uwe mke na mume.Lakini ukweli mwingine ni kwamba walio wengi hushindwa kufikia malengo na kuishia kusikojulikana kwa kila mtu kuwa na maisha yake na kubakiza stori tu.
KUAMBULIA PATUPU
Sehemu kubwa ya watu ambao wamekuwa wakiwasomesha wapenzi wao wamekuwa wakiingia mkenge baada ya mwanamke au mwanaume kupata msomi mwenzake na kumuona aliyemsaidia kufikia hapo si lolote bila kujali kama amesoma au lah.Kuna uwezekano kabisa wa kumpenda mpenzi wako na kuamua kujitolea kumsomesha kwa sababu hana uwezo, familia yake duni, yatima au umeamua tu kumkampani mpenzi wako, kwa maana ya ‘kushoo lavu’ kwake, lakini baada ya muda unakuja kusikia mpenzi wako anatoka na f’lani. Au yeye mwenyewe kwa jicho kavu, anaamua kukutolea uvivu na kukupa laivu kuwa: “Samahani f’lani, najua nimekupotezea muda wako sana, ninashukuru kwa upendo wako. Kwa kunisomesha na kunifikisha hapa nilipo. Lakini nasikitika kusema kuwa mimi si taipu yako, nimepata mtu ambaye ninaendana naye. “Ninakushauri na wewe utafute mwanamke au mwanaume ambaye unaendana naye. Kama hutajali ninaweza kukulipa gharama zako. Sorry!”
KEJELI NA DHARAU
Katika muktadha huu, kuna baadhi ya wengine ambao walijitolea kuwasomesha wapenzi wao ambao walijikuta wakiishia kukejeliwa na wapenzi wao wenyewe au ‘watu baki’ na wakati mwingine hudharaulika na kuonekana huna maana, limbukeni wa mapenzi na maneno mengine mengi kama hayo yanayolenga kuonesha kuwa ulibugi.Hakika inauma, inasikitisha, inakwaza, inakera, inakosesha usingizi na kukondesha kuona mnazi ulioumwagia maji na mbolea, ukitegemea mwisho wa siku ule nazi zake, leo umepata mkwezi mwingine. Unaweza kuwaza mambo mengi mabaya, lakini mwisho wa siku, huo ndiyo ukweli kuwa unakuwa umeliwa.
USHAURI WANGU
Unapochukua jukumu la kumsomesha mpenzi wako, fahamu yote mawili, kufanikiwa au kuingia mkenge kisha jiulize kama unamsomesha kama mpenzi wako unayetarajia awe mwandani wako au unamsomesha kama mtu baki na kama ikitokea ukafanikiwa kumuoa au kuolewa naye basi hewala. Lakini ukiweka nia moja tu ya kuwa unamsomesha Jeniffer ili baadaye uje umuoe, basi andika kuwa uwezekano wa kulia na kung’atwa upo, tena mkubwa sana.Hapa ninajaribu kukupa somo hili ili upate kujua faida na madhara ya kumsomesha mtu ambaye una ndoto ya kuwa naye maishani mwako. Kutokana na maisha na changamoto hizo za kimapenzi unapaswa kupima ili usije ukamsomesha mtu ambaye wewe ndiye unafikiria awe mkeo au mumeo, wakati yeye hana mawazo hayo.
Unachofanya wewe ni kutumia uwezo wako wa mali kumshawishi kwa kumsomesha kwa kuamini labda utafanikiwa kumnasa. Kwa leo ningependa kuishia hapa, nikukaribishe wiki ijayo kwenye mada nyingine murua na yenye mafunzo makubwa ndani yake.
Kwa ushauri wa UHUSIANO na UJASIRIAMALI jiunge na Mi&u WhatsApp:+255679979785 au tufollow Insta@mimi_na_uhusiano, Facebook Page: Mimi na Uhusiano au tembeleawww.miminauhusiano.blogspot.com
Kwa ushauri wa UHUSIANO na UJASIRIAMALI jiunge na Mi&u WhatsApp:+255679979785 au tufollow Insta@mimi_na_uhusiano, Facebook Page: Mimi na Uhusiano au tembeleawww.miminauhusiano.blogspot.com
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.