Makosa tuliyofanya tukashindwa
kufaulu masomo, au tukafukuzwa kazi, au biashara zetu zikafa. Wakati uliopita
umebeba mengi na ndiyo umekufikisha hapo ulipo sasa. Maamuzi uliyofanya siku
zilizopita huko nyuma, ndiyo yamekufikisha hapo ulipo. Watu uliokuwa karibu nao
siku zilizopita, ndiyo wamekusaidia kujenga maisha uliyonayo sasa. Mawazo
uliyoruhusu yatawale akili yako siku za nyuma, ndiyo yamekaribisha kila
ulichonacho sasa kwenye maisha yako. Kwa kifupi upo hapo ulipo sasa, kwa sababu
ulichagua hivyo siku zilizopita. Najua utabisha kama bado unaamini wazazi wako
ndiyo wamekufikisha hapo, au serikali ndiyo imekufikisha hapo, ila usikate
tamaa, nitakuonesha namna ya kutoka hapo ulipo sasa muda siyo mrefu.
Mbili; wakati uliopo sasa.
Wakati mwingine ambao unao kwenye maisha yako, ni wakati uliopo sasa, wakati
huu, hivi unavyosoma hapa sasa, ndiyo wakati ambao unao. Huu ni wakati muhimu
sana kwa sababu ndiyo unatengeneza kesho yako. Kama tulivyoona kwenye wakati
uliopita, ndiyo umetengeneza wakati uliopo sasa, wakati ulionao sasa ndiyo
unatengeneza wakati ujao. Kila unachofanya sasa, hapo ulipo unatengeneza
matokeo ya kesho. Namna unavyofanya kazi au biashara yako, ndiyo mbegu
unayoipanda kwa ajili ya kesho. Mawazo unayoruhusu yatawale akili yako sasa,
ndiyo yanatengeneza kesho yako. Na hata watu wanaokuzunguka sasa, ndiyo
wanakusaidia kuijenga kesho yako. Chochote unachofanya sasa, hakitaenda bure,
bali kitaijenga kesho yako, iwe ni kitu kizuri au kibaya.
Tatu; wakati ujao.
Huu ni wakati ambao bado hatujaufikia, ni wakati ambao unakuja, na hatuna
uhakika utakuwaje wakati huo. Hakuna mtu yeyote amewahi kufanikiwa kutabiri kwa
uhakika wa asilimia 100 kwamba wakati unaokuja utakuwaje. Hakuna ambaye amewahi
kuiona kesho, lakini tuna matumaini itakuwa bora, na mambo yatakuwa kama sasa
au bora zaidi. Wakati ujao ni matumaini kwetu, ndiyo unaotusukuma tuweke juhudi
zaidi leo, ili wakati huo uwe bora sana. Ndiyo maana tunakazana kuwekeza,
kuweka akiba na mengine ili kuhakikisha kesho, kwa vyovyote itakavyokuja, basi
tutaendelea kuwa vizuri. Kesho inatusukuma kuchukua hatua leo, ili inapokuja, tusiwe
kwenye wakati mgumu.

Tatizo kubwa tunaanza kulitengeneza hivi.
Sasa lipo tatizo kubwa sana kwenye hizi nyakati tatu, tumekuwa hatuziishi kama
ambavyo tumezielezea hapo juu, kwamba nyakati zilizopita ni jana, wakati uliopo
ni leo na wakati ujao ni kesho. Badala yake tumekuwa tunavuruga kila wakati na
mbaya zaidi kujinyima wakati wa kuishi ni sasa.
Picha huwa linaanza pale tunapofikiria wakati uliopita, makosa ambayo
tumefanya, fursa ambazo tumezikosa, na kujiona kama tumepoteza sana.
Tunajilaumu kwa nini tulifanya au hatukufanya kitu fulani. Tunajitesa kwa
makosa tuliyoyafanya huko nyuma. Na yote haya, tunayafanya kwenye wakati
tulionao sasa, ambao tulipaswa kufanya mambo ya sasa.
Hatuishii hapo, bali tunaiangalia na kesho pia, wakati ujao. Tunaangalia wakati
huo kwa hofu kubwa, tukiona mambo yatazidi kuwa mabaya, hali itazidi
kuharibika, maisha yatazidi kuwa magumu na hatutaweza tena kupiga hatua.
Tunajenga picha moja mbaya na ya hatari sana, picha inayotufanya tushindwe
kabisa kupiga hatua yoyote ile, na kubaki kama tumepingwa sindano ya ganzi.
Hili linachangia zaidi kuharibu wakati tuliopo sasa.
Kwa kuchanganya yale tuliyofanya au kutokufanya wakati uliopita, na kufikiria
mabaya zaidi kwa wakati ujao, tunajikuta hata wakati tulionao sasa hatufanyi
chochote. Hatuchukui hatua yoyote ambayo ingeweza kubadili hali ya mambo hapo
kesho, badala yake tunajaza akili yetu mawazo ambayo hayawezi kutusaidia.
Mawazo ambayo yanatupa hofu zaidi ya kufanya, na tunabaki hatujui tufanye nini.
Hapa ndipo wengi hukata tamaa na hata wengine kufikia kukatisha uhai wao.
Ipo njia ya kuhakikisha kesho yako inakuwa na mafanikio makubwa.
Na njia hiyo siyo ngumu kama unavyofikiri, bali ni rahisi sana, na ni kuchagua
kuishi leo.
Kwenye njia hii, unachagua kuishi leo, kwa sababu kile unachofanya leo ndiyo
kinaandaa kesho yako. Kwa njia hii unatambua yale yaliyopita, lakini unakubali
kwamba haijalishi utafanya nini, huwezi kubadili chochote ambacho kimepita,
huwezi kurudi na kufuta makosa yaliyopelekea kufeli, kufukuzwa kazi au biashara
kufa. Huwezi kurudi nyuma na kuzichukua zile fursa ambazo zilikupita. Lakini
unajua kwamba kwa kufanya kitu leo, kwa kuchukua hatua leo, basi unaitengeneza
kesho yako vizuri zaidi. Unachofanya kwa wakati uliopita ni kujifunza na
kusonga mbele.
Pia kwa wakati ujao, ambao tumekuwa tunautengenezea hofu, tunakubali kwamba
hatuwezi kuujua kwa uhakika, na hatuwezi kuuishi kabla haujafika. Hivyo
kupoteza muda mwingi kuufikiria kwa hofu, hakutatusaidia lolote kwa sasa. Hivyo
tunautumia kama hamasa ya sisi kufanya kitu leo.
Kazi kubwa kwetu ni kuishi kwenye wakati tuliopo sasa, kuchukua hatua kwenye
wakati huu, kufanya kitu sasa. Kuyaangalia kwa kina mawazo ambayo tumeruhusu
yatawale akili yetu sasa, je ni mawazo yanayotujenga au kutubomoa? Ni mawazo
chanya au hasi? Pia tuangalie wale ambao wanatuzunguka, je kuna mahali popote
wanaenda na maisha yao au wapo wapo tu. Ni watu ambao wana msaada kwetu au
wanaturudisha nyuma? Ni muhimu pia kuangalia kila jambo unalofanya sasa, kila
hatua unayopiga sasa na kuona kama ina mchango wowote kwenye kuyafanya maisha
yako kuwa bora zaidi leo na siku zijazo.
Namna unavyofanya kazi yako na hata biashara yako, je inaongeza ufanisi
zaidi?
Unatengeneza thamani zaidi?
Ili kuishi vizuri leo, na kuweza kuitengeneza kesho ambayo ni bora zaidi, basi
zingatia yafuatayo;
1. Kuwa na maono makubwa ya siku zijazo, mwaka mmoja kutoka sasa, miaka mitano,
miaka kumi na kuendelea. Siyo lazima uyafikie kama yalivyo, lakini yatakusukuma
kuchukua hatua.
2. Hakikisha kuna hatua unachukua leo, ambayo itakufanya kuwa bora zaidi ya
ulivyokuwa jana.
3. Usikubali kuzungukwa na watu ambao hawajui wapi wanakwenda, kaa mbali na
watu hasi.
4. Usipoteze muda wako kujutia makosa uliyofanya huko nyuma, au fursa ambazo
hukuzichukua.
5. Tumia muda wako wa leo vizuri, usipoteze hata dakika moja, poteza fedha
utazipata nyingine, poteza muda na hautaupata tena.
Fanya haya rafiki, na kesho yako, kwa hakika haitakuwa kama ilivyo leo, au
ilivyokuwa jana. Japo huwezi kujua kwa hakika itakuwaje, lakini itakuwa bora
zaidi.
BY Tatu Kiondo