DODOMA: Mbunge wa Jimbo la Kibamba, John Mnyika leo alisababisha kuzaazaa Bungeni Dodoma baada ya kugoma kutoka nje ya Bunge alipoamuriwa na Spika Job Ndugai kutokana na kile kilichodaiwa kukataa kuketi kama alivyoamuriwa na kiongozi huyo wakati mijadala ikiendelea.
Chokochoko hizo ziliibuka baada ya Mbunge wa Mvumi, Livingstone Lusinde kudai kwamba wapinzani bungeni humo wanatetea wezi wa mchanga wa dhahabu.
Mnyika ilibidi asimame na kutoa mwongozo kwa kusema wao wapinzani sio wezi isipokuwa walichokuwa wakikisema ni kulalamikia mikataba mibovu ya madini ambayo imeingiwa na serikali na kusababisha kufikia hapa tulipo.
Wakati Mnyika akiendelea kumpa taarifa Lusinde, mbunge ambaye hajajulikana jina alisikika akisema kwa sauti ‘mwizi’, hali iliyomfanya Mnyika kumuomba spika amjuwe aliyemuita mwizi, hata hivyo, Spika Ndugai akawa anamsisitizia akae chini.
Alimuomba kukaa chini mara tatu lakini Mnyika hakutii ndipo Ndugai alipomuamuru atoke nje lakini pia hakutoka, hivyo akawaita askari wa bunge aliowaamuru waingie ndani na kumtoa nje kwa nguvu mbunge huyo kijana.
Kuona hivyo Mbunge wa Kawe, Halima Mdee na yule wa Bunda, Ester Bulaya, waliingilia kati kuwazuia askari wa bunge kumtoa nje Mnyika, hali iliyoleta tafrani, hata hivyo, alitolewa na kwenye lango la kuingilia bungeni, alisukumwa na ‘kutupwa’ nje ya mjengo.
Spika alitangaza kumsimamisha Mnyika asihudhurie vikao vya bunge kwa wiki moja huku Ester Bulaya na Halima Mdee akisema wataandikiwa barua ili wakahojiwe na Kamati ya Haki na Maadili ya Bunge.
Kwa Ushauri Wa Mahusiano, Mada Za Mahaba, Hadithi, Machombezo, Mikasa Ya Kweli Ya Mapenzi Na Ujasiriamali. Jiunge na M&U SMS au M&U WhatsApp kupitia Na. 0679979785.
Pia tembelea www.miminauhusiano.blogspot.com, Insta:@mimi_na_uhusiano au tembelea ukurasa wetu wa Mimi na Uhusiano kwa ku-Bonyeza Hapa