DENTI ATOROSHWA, AWEKWA KINYUMBA
Boniphace Ngumije
Dunia imekwisha! Binti mwenye umri wa miaka
14 (jina linahifadhiwa kimaadili), mkazi wa Majohe-Kwawarioba, Gongo la Mboto
jijini Dar ambaye ni mwanafunzi (denti) wa kidato cha kwanza katika shule moja
ya sekondari iliyopo maeneo hayo, anadaiwa kutoroshwa nyumbani kisha kuwekwa kinyumba.
Kwa mujibu wa mama mzazi wa denti huyo,
Edna Zacharia, tukio hilo lilijiri hivi karibuni ambapo juhudi zote
alizozifanya kumtafuta mwanaye huyo ziligonga mwamba huku tetesi za mhusika
aliyetenda tukio hilo akiwa nazo.
Binti huyo anayedaiwa kuwekwa kinyumba.
Mzazi huyo alisema kuwa binti yake huyo
alianza kufanya jaribio la kutoroka siku moja kabla ya kutimiza azma yake ambapo
tofauti na utaratibu wa kawaida, siku hiyo alirejea nyumbani kwa
kujifichaficha.
Mama huyo aliendelea kueleza kwamba, baada
ya kumhoji mwanaye, alimwambia alikuwa amepoteza shilingi 500 ya mama huyo,
hivyo aliogopa kuonekana mbele yake akihofia kupewa adhabu.
Alisema alimsamehe mwanaye na akamwambia
aende kulala na mdogo wake lakini kwa kuwa azma yake ilikuwa kutoroka, siku
iliyofuata mama huyo aliporejea kutoka kwenye majukumu yake, hakumkuta na
baadhi ya nguo zake hazikuonekana.
“Baada ya saa 24 niliripoti tukio hilo
kwenye Kituo cha Polisi cha Majohe, nikaandikisha taarifa, tukaanza kumsaka
usiku na mchana nikisaidiana na ndugu zangu, tulipata taarifa kuwa yupo kwa
kijana muuza mkaa anayefahamika kwa jina la Issa anayeishi Mabibo-External
(Dar), tukaenda polisi na kufunguliwa jalada namba STK/RB/1835/15 -KUTOROSHA
BINTI CHINI YA HIMAYA YA WAZAZI),” alisema mama huyo.
Edna alisema katika harakati za kumtafuta
mwanaye huyo, aliwataarifu baadhi ya ndugu zake akiwemo kaka yake, Damian
Ndelwa ambaye mkewe ndiye alikuwa anafahamu mahali alipoonekana binti huyo,
ndipo wakakusanyana na baadhi ya watu wake wa karibu kisha kwenda kuvamia
kwenye eneo la tukio.
Hata hivyo, mtuhumiwa na denti huyo
walikimbia ndipo ndugu hao wakachukua uamuzi wa kwenda kituo cha polisi
kilichopo karibu walikoambiwa waendelee kumtafuta kwa kuwa wana RB.
Kuhusu shuleni, Edna alisema mwalimu mkuu
na walimu wengine walimshauri kwenda kutafuta msaada kwenye taasisi ya haki na
sheria lakini alidai alipofika huko walimrudisha polisi wakimsisitiza kuendelea
kumtafuta na kuripoti polisi ikiwa hatapatikana.
Mama huyo aliwaomba watu watakaomuona
wawasiliane naye kupitia namba za simu zake za mkononi 0788 291 318, 0769 737
447 au 0672 506 746 au watoe taarifa kwenye kituo cha polisi kilichopo karibu.
Imewekwa
na Timotheo Mjuni;M&U
Chanzo:GPL
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.