Mafanikio ya biashara hayatokani na kuwa na wazo bora na mtaji pekee. Wengi wamekuwa wakifikiria vitu hivi viwili kabla ya kuanza biashara na hata wanapoanza biashara. Ambacho wengi hawaangalii ni kwamba kuna watu ambao wamekuwa na mawazo mazuri sana ya kibiashara, na wakawa na mtaji mkubwa pamoja na watu waliopo tayari kuwekeza kwenye biashara zao. Lakini watu hao wameshindwa vibaya sana kwenye biashara walizojaribu kufanya.
Watu hawa wamekuwa na kila kitu tunachoamini kinahitajika ili biashara kukua, wazo bora, mtaji mkubwa pamoja na mtandao mzuri. Vitu vyote hivyo vinafanya kazi vizuri lakini matokeo yanakuwa tofauti na wengi walivyotarajia. Je hapa tatizo linatokea wapi? Ni bahati mbaya? Au watu wanachezewa michezo ambayo siyo mizuri? Matatizo mengi kwenye biashara huwa yanaanzia kwenye msingi na falsafa ya biashara yenyewe. Misingi hii inawekwa na mwanzilishi wa biashara na inatakiwa kusimamiwa na kila mtu anayekuwepo kwenye biashara ile. Tatizo la biashara nyingi ni kwamba hakuna misingi iliyo wazi na hivyo kila mtu kwenye biashara ile anafanya maamuzi yake mwenyewe. Na hata pale ambapo misingi ipo, siyo wote wanaifahamu na kuitumia kwenye maamuzi ya kila siku
Biashara yoyote kama yalivyo maisha, ili iweze kufanikiwa, inahitaji kuwa na misingi ambayo inafuatwa. Inahitaji kuwa na falsafa ambayo watu wote kwenye biashara wanaiamini na hata wateja wanaiamini. Biashara isiyokuwa na misingi na falsafa, haiwezi kudumu muda mrefu, kwa sababu itafika wakati wa changamoto, watu watafanya maamuzi mabovu na yataigharamu biashara. Pia wateja wanashindwa kujua biashara inasimamia nini, kwa sababu kila wakati wanapata huduma tofauti. Wateja wanapokosa msimamo kwenye biashara hawajisikii amani kuendelea kupata mahitaji yao kwenye biashara ile.
Wewe kama mfanyabiashara unahitaji kujijengea misingi na falsafa ya biashara yako, ukishakuwa na misingi hii hakikisha kila anayehusika kwenye biashara anaijua na kuisimamia wakati wote. Pia hakikisha wateja wananufaika kupitia msingi na falsafa hiyo na kuhamasika kuendelea kufanya biashara na wewe.
Misingi ya biashara ni nini?
Misingi ya biashara ni vile vitu ambavyo biashara inasimamia, vile vitu ambavyo ni lazima biashara yako ifanye kwa mteja. Pia kuna vitu ambavyo ni mwiko kwa biashara yako kufanya. Misingi hii ndiyo itakayoweza kutoa utatuzi pale ambapo kuna changamoto kwenye biashara yako. Misingi ndiyo inawawezesha watu waliopo kwenye biashara yako kuweza kufanya maamuzi sahihi hata pale ambapo wanakuwa hawana taarifa za kutosha.
Baadhi ya misingi muhimu unayohitaji kujijengea kwenye biashara ni uaminifu, uadilifu, kuweka maslahi ya mteja mbele na kwenda hatua ya ziada katika kumhudumia mteja. Misingi ya biashara inatofautiana kulingana na aina ya biashara na malengo ya mfanyabiashara mwenyewe.
Falsafa ya biashara ni nini?
Watu wengi wakisikia falsafa wanaogopa na kuona ni kitu kigumu, wanaona ni kitu cha kwenda kusomea ili kuwa na imani fulani. Lakini huo siyo ukweli, falsafa ni kile kitu ambacho mtu anasimamia. Ile sababu ambayo inawafanya watu kufanya kile ambacho wanafanya licha ya kuwepo na vitu vingine vya kufanya. Falsafa yako kibiashara ndiyo inayowafanya wateja waje kununua kwako licha ya kuwepo kwa wafanyabiashara wengine kama wewe. Falsafa ndiyo inayokuwezesha kumudu ushindani mkali ulipo kwenye biashara unayofanya.
Ili kuweza kujenga falsafa ya biashara yako, unahitaji kujua KWA NINI biashara yako ipo. Ni changamoto gani, au mahitaji gani ya wateja ambayo biashara yako inatimiza. Kama biashara yako itaondoka leo ni kitu gani kikubwa ambacho watu watakikosa. Jua hili na mambo yako yote kwenye biashara yawe yanasaidia hilo. Jenga falsafa ya biashara yako ambayo itamwezesha mteja kuwa na uhakika kila anapofanya biashara na wewe. Falsafa ya biashara haijengwi kwa kushusha bei au kwa kutoa ofa, wala falsafa haijengwi kwa kuwapa wateja hofu. Bali falsafa ya biashara inajengwa kwa kuwafanya watu waamini kile unachofanya, kwa sababu kina manufaa kwako. Angalia biashara yako inawasaidiaje watu na fanya hilo kuwa dhumuni kuu la biashara yako.
Usifanye biashara kwa mazoea, kwamba umeona fursa, fedha unazo na wazo umelipata, bali tengeneza biashara itakayodumu kwa muda mrefu kwa sababu ina misingi na falsafa. Pia usiwe tu na falsafa na misingi kwenye makaratasi, bali vifanye vitu hivi kuwa maisha ya biashara yako kila siku, kwa kuvifanyia kazi kila siku kwenye biashara yako.
Kwa Ushauri Wa Mahusiano, Mada Za Mahaba, Hadithi, Machombezo, Mikasa Ya Kweli Ya Mapenzi Na Ujasiriamali. Jiunge na M&U SMS au M&U WhatsApp kupitia Na. 0679979785.
Pia tembelea www.miminauhusiano.blogspot.com, Insta:@mimi_na_uhusiano au tembelea ukurasa wetu wa Mimi na Uhusiano kwa ku-Bonyeza Hapa
BY TATU KIONDO