Saturday, July 1, 2017

Published 7/01/2017 03:07:00 PM by

CHANGAMOTO KATIKA BIASHARA


Biashara zina changamoto, lakini pale mfanyabiashara mwenyewe anaongeza changamoto, biashara inakuwa ngumu zaidi. Wafanyabiashara wengi wamekuwa wakitengeneza changamoto nyingi kwenye biashara zao wao wenyewe na hivyo kujizuia wao wenyewe kufanikiwa. Hii ni sawa mtu anaendesha gari, huku amekanyaga mafuta na breki kwa wakati mmoja. Atatumia mafuta ya kutosha lakini hatafika popote.

1.  Kutaka kurahisisha biashara.
Nimekuwa naona wafanyabiashara wengi, hasa wanaoanza wanapojaribu kukwepa kufanya kazi zao. Wengi wamekuwa wanafikiri kwa kumiliki biashara zao, basi hakuna wa kuwapangia wafanye nini na kwa wakati gani. Hivyo hujiona kama mabosi ambao kazi yao ni kuwatuma watu wengine. Kwa njia hii wamekuwa wakijikuta wanapata changamoto nyingi kama za wasaidizi kuharibu biashara, wateja kupata huduma mbovu na hata mzunguko wa fedha kutokuwa mzuri.
Kitu unachopaswa kujua ni kwamba, biashara yako inakutegemea sana wewe, lazima uwe karibu sana na biashara yako, lazima ujue kila kinachoendelea kwenye biashara yako. Na hapo unaweza kuchukua hatua sahihi kabla mambo hayajaharibika zaidi. Usitake kurahisisha biashara, usitafute ubosi wa haraka, endesha biashara yako vizuri, kaa nayo karibu na jua kila kitu.

2. Kuchanganya matumizi ya kawaida na fedha za biashara.
Hii ni changamoto moja kubwa ambayo inaua biashara nyingi ndogo. Kabla hata hatujaenda mbali sana, wewe jaribu tu kuangalia biashara nyingi za nyumbani, labda duka linalofunguliwa nyumbani ambalo ni la mahitaji muhimu. Huwa ni biashara ambazo wengi hawaoni faida. Tena wapo ambao wamekuwa wanafungua na kufunga biashara hizo mara kwa mara.
Kushindwa kutenganisha au kutofautisha matumizi ya kawaida na fedha binafsi, kunawafanya wafanyabiashara kutengeneza changamoto ya mzunguko wa fedha kwenye biashara. Hii ni kwa sababu fedha nyingi inaondoka kwenye biashara na hivyo biashara kushindwa kujiendesha yenyewe.
Unapokuwa kwenye biashara, jua kabisa kwamba wewe na biashara yako ni vitu viwili tofauti kabisa, ndiyo biashara ni yako, lakini siyo wewe. Hivyo mambo ya biashara lazima yawe chini ya biashara, na mambo yako binafsi lazima yawe chini yako. Usichanganye mambo haya, kila kitu kiende kwa kumbukumbu.

3. Kuajiri watu wasio na sifa au uwezo wa kufanya kazi kwenye biashara.
Hii ni changamoto nyingine ambayo wafanyabiashara wenyewe wamekuwa wanaitengeneza. Wafanyabiashara wengi wadogo na wa kati, inapofika wakati wa kuajiri, huangalia watu wanaoweza kuwaajiri na kuwalipa kiasi kidogo cha fedha. Na kama unavyojua, watu ambao wapo tayari kulipwa kiasi kidogo cha fedha, ni watu ambao hawana kitu kingine cha kufanya. Sasa kama mtu hana kitu kingine anaweza kufanya, unafikiri ataweza kuwa wa msaada kwenye biashara yako?
Unapopanga kuajiri wasaidizi kwenye biashara yako, angalia watu wenye sifa zinazoendana na kazi unayopanga kuwapa. Pia wawe na uwezo wa kutekeleza majukumu unayowapangia kufanya. Hata kama huna uwezo wa kuwalipa kiasi kikubwa, kuwapata watu hao unaweza kuona namna gani wanaweza kunufaika zaidi kupitia wewe.


4. Kukopesha wateja bidhaa au huduma.
Hii pia ni changamoto ambayo mfanyabiashara mwenyewe anajitengenezea. Anajikuta akiwapa wateja bidhaa au huduma kwa mkopo, kwa ahadi ya kulipwa baadaye. Lakini kinachotokea ni kwamba baadhi ya wanaokopa wanakuwa siyo waaminifu na hivyo fedha hazilipwi kwa wakati. Jambo hili huathiri mzunguko wa fedha kwenye biashara na kupelekea biashara kuyumba na hata kufa.
Usitengeneze utamaduni wa kukopesha kwenye biashara yako. Hata kama wengine wanafanya hivyo, wewe tengeneza wateja watakaoipenda na kuiheshimu biashara yako kiasi cha wao kuwa tayari kulipa pale wanapofanya manunuzi.

5. Kutafuta faida ya haraka.
Wafanyabiashara pia wamekuwa wakihadaika na njia za kupata faida ya haraka kwa muda mfupi. Lakini njia hizo zimekuwa haziwaachi salama, hasa baada ya muda wa faidia kuisha. Wengi wanajikuta wameingia kwenye mambo yanayoharibu sifa zao au hata kuvunja sheria. Kwa njia hii biashara inashindwa kwenda.
Unapokuwa kwenye biashara, epuka kabisa kutafuta njia ya mkato. Ijue misingi ya mafanikio kwenye biashara, na ifuate misingi hiyo. Kitu chochote nje ya msingi, achana nacho, hata kama kila mtu anafanya.
Acha mara moja kutengeneza changamoto kwenye biashara yako, biashara yenyewe ni changamoto, kuongeza nyingine ni kutengeneza njia ya uhakika ya kushindwa kwenye biashara.

 # u & me 
      edit