Nina
mke na mtoto mmoja. Kwa sasa nimeajiriwa kama mhasibu msaidizi katika
kampuni moja hapa Dar es Salaam. Mwaka mmoja baada ya ajira niliamua
kujiunga na masomo ya CPA ili kuongeza thamani ya taaluma yangu ya
uhasibu. Changamoto yangu kipato hakitoshi masomo magumu na yanachukua
muda zaidi kutokana muda mwingi kuwa ofisini. Hivyo nafikiria kuachana
na masomo na hiyo fedha ambayo naiwekeza kwenye masomo ya CPA nafikiria
niiwekeze kwenye biashara ingawa natamani kuendelea na masomo ya CPA.
Naomba ushauri maana naona umri unazidi kwenda (nina miaka 33) niachane
na CPA na kutafuta biashara ya kufanya na kuweka juhudi zaidi huko?
Ahsnte –
Pole
sana kwa changamoto hiyo unayopitia. Ni wakati mgumu sana uliopo, kama
umeajiriwa, una familia, kipato kidogo na kama hayo hayatoshi, una
masomo magumu ambayo pia yanakugharimu.
Ni
wakati mgumu sana, lakini kabla ya kufanya maamuzi yoyote, lazima ukae
chini na kutafakari kwa makini maisha yako na ndoto zako kubwa, yapi
maono ya maisha yako, kupanga vipaumbele vyako vizuri na kisha kuweka
mkakati ambao utaufanyia kazi, kwa nidhamu ya hali ya juu sana.
Hivyo,
kabla hujafanyia kazi ushauri ambao nitakupa hapa, kaa chini kwanza
uangalie maisha yako na maono yako. Kisha angalia hatua mbayo
utaichukua.
Baada ya hayo, ushauri wangu ninaokupa ni huu; FANYA VYOTE KWA PAMOJA.
Ndiyo,
namaanisha ufanye vitu vyote hivyo kwa pamoja. Yaani una familia,
umeajiriwa, una masomo na unafikiria kuhusu biashara. Badala ya kutaka
kuacha masomo ili ufanye biashara, fanya masomo na fanya biashara.
Huenda hukutegemea jibu hili na huenda una wasiwasi haiwezekani, lakini
nakuambia inawezekana kama kweli utaamua liwezekane.
Nina
amini masomo yako ya CPA hayatachukua zaidi ya miaka mitatu, hivyo basi
rafiki, nataka ujitangazie miaka mitatu ya vita. Hii inakwenda kuwa
miaka mitatu ya tofauti kabisa kwenye maisha yako, miaka mitatu ya
kuyajenga upya maisha yako.
Kwenye
miaka hii mitatu, jipe ruhusa kabisa ya kwenda kinyume na maisha yote
ya kijamii, kwa sababu jukumu lililopo mbele yako siyo dogo, ni kubwa
sana, hivyo linakuhitaji na wewe uwe na maamuzi ambayo wengine
hawatakuelewa.
Kwa
uzoefu wangu binafsi na kupitia watu ambao nimewashauri, nimekuja
kugundua karibu kila mmoja wetu ana uzembe fulani ambao unamrudisha
nyuma. Licha kweli ya maisha kuwa magumu, kipato kidogo na kazi kuwa
nyingi, bado tuna uzembe ambao tunaufanya, na uzembe huu unaturudisha
nyuma.
Kwa
mfano, utakuta mtu pamoja na changamoto alizonazo, bado anapata muda wa
kuangalia tv, kusoma magazeti, kusikiliza redio. Bado ana muda wa
kufuatilia mpira, anakaa kabisa chini dakika 90 kuangalia mpira. Bado
ana marafiki anaokutana nao jioni na wanakaa kupiga stori, labda
wakipata vinywaji. Mtu huyu huyu yupo kwenye mitandao ya kijamii,
analala muda wa zaidi ya masaa sita. Mtu huyo unakuta siku za kazi ni
tano, jumatatu mpaka ijumaa, na jumamosi labda nusu siku, halafu
jumapili anapumzika. Mtu huyo huyo ana mambo mengi ambayo yanampotezea
fedha lakini hakuna hatua anazochukua. Na mambo yanapokwenda hivi,
lazima maisha yazidi kuwa magumu.
Hivyo hatua za kuchukua ni hizi;
- Badili kabisa mfumo wako wa maisha.
Tenga
miaka hiyo mitatu kama nilivyokueleza hapo juu, miaka hiyo hakikisha
unaimaliza cpa, unaongeza kipato chako kupitia biashara, na kuimarisha
maisha yako.
Weka
thamani kubwa sana kwenye muda wako, usipoteze hata dakika yako moja.
Punguza watu na mambo mengine yoyote ambayo siyo muhimu kwako. Kama kuna
mtu ambaye hatakuelewa kwa mabadiliko ya maisha utakayofanya, siyo
muhimu, achana naye. Kaa na wale watu wanaoelewa unakoenda, na
wanakuunga mkono na kukusaidia. Achana na watakaokukatisha tamaa, na kwa
taarifa tu, watakuwa wengi.
- Chagua biashara ambayo utaifanya.
Chagua
biashara ambayo unaweza kuifanya, kwa kuanzia hapo ulipo sasa. Na kwa
kuwa muda wako ni mdogo, nakushauri uanzishe biashara ya huduma, ambapo
utatoa ulichonacho kwa wengine.
Kwa mfano wewe umesema ni mhasibu, sasa angalia unawezaje kutumia uhasibu wako kama huduma na kuiuza kwa wengine.
Je unaweza kuwasaidia wafanyabiashara wadogo na wa kati kuandaa mahesabu ya biashara zao?
Je unaweza kupata kazi ya muda wa ziada kazini kwako au sehemu nyingine ambayo unaweza kutoa thamani zaidi?
Je unaweza kutoa huduma ya kuwafundisha watu wengine wanaojifunza uhasibu au kitu kingine ambacho unaweza kufundisha?
Je unaweza kuanzisha biashara nyingine ndogo ukapata mtu wa kuifanya kwa karibu na wewe ukapata muda wa kuifuatilia kila siku?
Endelea
kujiuliza maswali hayo, kulingana na mazingira yako mpaka upate jibu
lenye kuweza kufanyika. Lazima upate jibu na kuanza kulifanyia kazi
mapema.
- Panga ratiba ya kila siku ambayo utaisimamia vizuri.
Kitu
muhimu sana ambacho unapaswa kufanya, ni kupangilia ratiba yako ya kila
siku. Na anza na mpango wa siku ambao una mambo utakayoyafanya kila
siku. Kwa mfano kwako wewe, kazi, masomo, biashara na familia ni mambo
ambayo lazima uyafanye kila siku.
Hivyo hakikisha kila siku ya kazi, unatenga muda ambao utakuwa wa kufanya kazi.
Katika
siku nyingine zote za wiki, panga muda wa kusoma masomo yako, na pia
panga muda wa kufanya kazi kwenye biashara yako. Hili ni kila siku,
kumbuka kwa sasa huna siku ya mapumziko, utaendesha maisha yako siku
saba za wiki, na siku ambayo huendi kazini ndiyo unazitumia vizuri
zaidi.
Panga
kuamka mapema kuliko ulivyozoea, aka masaa mawili au hata moja kabla ya
muda wako wa kawaida wa kuamka. Na muda huo utumie kusoma, kila siku.
Unapokuwa kazini, muda wowote unaopata wa mapumziko, usiupoteze, badala
yake utumie kusoma. Jioni ukitoka kazini, usipoteze muda, weka muda huo
kwenye biashara yako.
Kusoma
na biashara vikweke kwenye ratiba yako ya kila siku. Najua watu wengi
huwa hawasomi mpaka mitihani ikaribie, wewe usiwe mtu wa aina hii.
Kuanzia siku ya kwanza unapojiandikisha na masomo na kupata mtaala,
panga ratiba ya kila siku utasoma nini mpaka unapofikia wakati wa
mtihani. Kwa njia hii utakuwa na maandalizi mazuri na mambo yako mengine
yataenda. Kama ukiweza kujijengea nidhamu, unaweza kuweka muda wako
kwenye kujisomea mwenyewe na kuepuka kuhudhuria madarasa ambayo
yatakuhitaji kulipa fedha zaidi.
- Jenga nidhamu ya hali ya juu sana, mambo hayatakuwa rahisi.
Kusoma
hapa itakuwa rahisi, na unaweza ukaona eh, nitafanya hivi. Lakini siku
ya kwanza kuanza kufanya tu, dunia yote itakupinga. Utafika wakati wa
kuamka na utajiambia kwa nini niamke leo, nitaamka kesho. Utafika kazini
na kupewa majukumu zaidi. Utapanga ratiba ya kusoma na kuona mtihani
bado upo mbali, utasoma tu.
Dunia
inakusubiri ikuangushe, hivyo jiandae vizuri sana, tena sana. Na
usikubali kwa namna yoyote ile kuvunja kile ulichopanga. Kwa lolote
linalotokea ambalo hukutegemea, jipange kuhakikisha mambo yako yanaenda
kama ulivyopanga.
Jambo
moja naweza kukuhakikishia ni kwamba, maisha yatakuwa magumu, lakini
kwa uhakika zaidi ni kwamba hutakufa, utazidi kuwa imara na maisha yako
yatakuwa bora zaidi.
Kwa Ushauri Wa Mahusiano, Mada Za Mahaba, Hadithi, Machombezo, Mikasa Ya Kweli Ya Mapenzi Na Ujasiriamali. Jiunge na M&U SMS au M&U WhatsApp kupitia Na. 0679979785.
Pia tembelea www.miminauhusiano.blogspot.com, Insta:@mimi_na_uhusiano au tembelea ukurasa wetu wa Mimi na Uhusiano kwa ku-Bonyeza Hapa
Na.Mi&u