Friday, January 29, 2016

Published 1/29/2016 10:25:00 PM by with 0 comment

HIVI MAPENZI YAMEKUFANYIA NINI?


Mpenzi msomaji wa safu hii M&U shukrani nyingi zikufikie kwa maoni na ushauri wako. Baada ya wiki iliyopita kukupa mbinu za kupigania penzi lako kwa maana ya kulia au kulisusa siyo dawa, wiki hii napenda nijue wewe msomaji wa makala hii. Mapenzi yamekufanyia nini?


Ninaamini kila mtu atakuwa na jibu kulingana na vile mapenzi yalivyomfanyia katika maisha yake ya uhusiano.
Kwa kuanza tu, wapo watu waliofika ughaibuni kwa sababu ya kuwa na wenza wa nchi husika na mwenza wake kumkaribisha au kuamua kuishi naye katika nchi hiyo.

Wapo walioumia kiasi cha kutotaka kusikia tena kitu kinachoitwa mapenzi wala mpenzi, wengine wameshindwa kuendelea na masomo baada ya kujiingiza katika uhusiano wa kimapenzi wakiwa na umri mdogo, jambo lililowasababishia kushindwa kumudu vitu viwili kwa wakati mmoja.


Wapo waliofanikiwa kupata watoto wazuri na wenye kuwasaidia katika maisha yao, lakini pia wapo waliopata watoto watukutu walioshindikana na wazazi wao, wanasubiri tu waadhibiwe au wafundishwe na ulimwengu.
Wengine wamepata mafanikio baada ya kupata watoto werevu ambao wanawasaidia katika maisha yao ya kila siku.
 
Wapo wengine walioambulia kupata magonjwa ya ziana na sugu kwa sababu ya mapenzi bila kusahau kuna wengine walipotea kwenye ramani ya dunia, kisa kikiwa ni mapenzi.
Bila kusahau wapo waliofungwa jela kwa kubaka, kuuwa au tukio lolote lililosababishwa na mapenzi.

Kwa jumla mapenzi yamesababisha mambo mengi sana kwenye jamii inayotuzunguka, cha msingi ni kujiuliza, je, mapenzi unataka yakufanyie nini? Yakuambukize magonjwa ya zinaa kisha yakuue, yakuning’inize, yakutese na kukuteketeza au yakupatie watoto na familia bora ili ufurahie maisha. 

Au yasababishe kuongezeka kwa watoto wa mitaani na wanaoishi katika mazingira magumu? Au yakugombanishe kazini na bosi wako, mke au mume wa bosi wako?
Au yakutenganishe na ndugu zako au uvuruge maisha yako kwa kupigwa au kumpa mimba mwanafunzi mwenzio? Unataka mapenzi yakufanyie nini? Tafakari!
Usikose wiki ijayo kwa mada nyingine. Pia usikose kutembelea ukurasa wetu wa Mimi na Uhusiano kwenye Facebook kwa ushauri na maswali kuhusu uhusiano.



      edit

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.