NIKUKARIBISHE mpenzi msomaji wa Blog yetu ya Mimi na
Uhusiano ‘M&U’ katika kuzungumzia
mada inayosema “PAMOJA NA MAUMIVU, HUWEZI KUYAEPUKA MAPENZI.”
Yawezekana umeumizwa na mapenzi na unatamani kuyaepuka, wakati
ukweli ni kwamba hayaepukiki moja kwa moja isipokuwa labda kwa muda.
Najua wengi mnaweza kushangaa lakini huo ndiyo kweli
wenyewe, pamoja na kuumizwa, kuteswa, kusimangwa, kutukanwa, kupigwa na
kufanyiwa vimbwanga vya kila aina kuhusiana na mapenzi, ukweli ni kwamba mapenzi
huwezi kuyaepuka moja kwa moja labda upoteze kabisa hamu na hisia juu ya
mapenzi, lakini naamini bado itatokea siku moja hisia zako zitanyanyuka tu.
Kwa wale walioshika dini mnaelewa kwamba, Mungu aliumba kila
kitu kwa makusudi maalum, ikiwa ni pamoja na kuujaza ulimwengu, mwanadamu wa
jinsi ya kike kumfurahisha wa jinsi ya kiume, vivyo hivyo kinyume chake.
Poleni sana wale wote wanaotamani kuyaepuka mapenzi,
akiwemo mmoja wa wasomaji aliyenitumia ujumbe mfupi akidai ameteswa sana na
mapenzi, kila mara amekuwa mtu wa kutokwa machozi, amekuwa mtu wa kukosa furaha
kiasi cha kutamani hata kujitoa roho, ila Mungu akamnusuru, akaamua kuomba
ushauri angalau aepukane na suala zima la mapenzi.
Mwanadamu ameumbwa na mihemko au hisia, kwa namna yoyote
ile unaweza kuvumilia kwa muda lakini kuna siku uvumilivu utakushinda. Ndiyo maana
hata vitabu vitakatifu vinaeleza kabisa kwamba kama unaweza kuvumilia, basi
vumilia ila kama huwezi basi oa na siyo kurukaruka kama wengi wanavyofanya kwa
sasa.
Watu wengi sana wamekuwa wakitamani kujiepusha na
mapenzi, wanatamani kukaa mbali kabisa na suala zima la uhusiano, kama ni
mwanamke, hataki au hapendi kuwa karibu na wanaume. Pia wapo wanaume wa namna
hiyo, ukiuliza utaambiwa, ‘nilishaumizwa sana, wanawake siyo watu na mwalimu
wao ni mmoja au wanaume wote ni sawa tu na mama yao ni mmoja kwa sababu tabia
zao ni zilezile’.
Ni kweli mapenzi yanaumiza sana lakini ukweli ni kwamba
pia huwezi kuyaepuka katika maisha yako ya uhai. Inawezekana kukaa kando kwa
muda lakini si kuepuka maumivu au misukosuko ya mapenzi. Sidhani kama kuna
uhusiano usiokuwa na mikwaruzo, sina imani kama kuna barabara ndefu isiyokuwa
na kona katika dunia hii. Pia sitaki kuamini kwamba kwenye maisha kuna watu
wanaofurahia maisha siku zote bila kuwa na chembe ya misuguano penzini.
Kwa taarifa yako, hata huyo unayemuona bosi mtaani au
mtu mzima, kuna wakati anateseka na kutokwa machozi kwa sababu ya mapenzi.
Chanzo-GPL
Tukutane
wiki ijayo kwa mada nyingine tamu, pia usikose kutembelea ukurasa wetu wa Mimi
na Uhusiano kwenye Mtandao wa Facebook, Instagram na unaweza kujiunga nasi
kwenye la WhatsApp kujua mengi kuhusu mapenzi.
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.