Ni Jumatatu nyingine tunakutana wanajamvi
wa XXLove katika kujifunza namna ya kukabiliana, kuzielewa na kuziishi
changamoto mbalimbali tunazokutana nazo kwenye uhusiano, lengo likiwa ni
kuboresha uhusiano huo na kuufanya uwe bora na wa kuigwa kwa mwaka huu wa 2016
na miaka mingine mingi tutakayojaliwa na Mwenyezi Mungu.
Wanawake wengi wamekuwa wakiwalalamikia
wapenzi wao kutokushinda nyumbani hasa siku za mapumziko, binafsi ninaamini
kutokushinda huko kwa wanaume majumbani mwao kunachangiwa na vitu vingi sana
ambavyo vinaweza kuwa ni vidogovidogo ila vyenye kukwaza.
Hakuna kitu kidogo, ila kizuri
kinachopendwa na wapenzi wengi, hasa wa kike kama mpenzi, mchumba au mume wake
kushinda nyumbani siku za mapumziko, wanawake wanapenda sana ‘kupetiwapetiwa,‘
wanapenda kupita mbele ya wenza wao wakijitingisha walivyojaliwa ili wenza wao
waone. Wanapenda kupata muda wa kuzungumza na wenza wao kuhusu maendeleo ya
familia yao japo kwa wiki mara moja na kuendelea.
Tatizo linaloonekana ni kwamba wanaume
wengi huwa hawako tayari kubaki nyumbani kwa muda mrefu, siku ya/za mapumziko
kwa kuhofia malumbano ya hapa na pale.
Wengine ni kwa sababu ya tabia za mwenza
wake (wewe mwanamke), anaamini kwa jinsi ulivyo akisema ashinde tu ndani basi
siku haiwezi kuisha bila kushikana shati au kutukanana, hivyo anaona bora
kwenda zake kwa washkaji au baa kula masanga ili akirudi nyumbani muda wa
migongoro na malumbano uwe angalau umepungua kidogo.
Ushauri wangu, angalia na rekebisha mapito
yako, jiulize ni nini? Tabia ipi? kero au karaha zipi kwa mwenza wako
zinazomfanya asishinde nyumbani au pengine ni tabia yako ya kidomodomo, gubu au
kisirani?
Ukiweza kujua vyanzo vinavyomfanya mwenza
wako asishinde nyumbani, itakuwa ni vizuri sana na kama utavifanyia kazi basi
naamini mapenzi yako kwa mwaka 2016 yatakuwa matamu mno na yenye furaha.
Ingawa siyo wote wanakimbia kero za wenza
wao, wanaume wengine ndiyo wanapopatia sababu ya kufanya mambo yao kama kula
masanga, kukutana na marafiki, kufanya dili zao za nje ya ofisi na hata
kuchepuka kwa wenye tabia hiyo.
Hebu fanya mwaka 2016 kuwa wa neema kwako,
kama ni mwanamke jirekebishe, nawe mwanaume badilisha baadhi ya tabia zako,
pengine ndizo chanzo kikubwa cha malumbano yenu yanayosababisha ninyi
kukwidana, kutengana nakadhalika.
Kwa kuzingatia na kuufanyia kazi upungufu
wenu ni hakika mtakuwa kama mnalipevusha upya penzi lenu, mwanamke badilisha
vijitabia vyako vya ajabu, mwanaume pia fanya utaratibu wa kupumzika nyumbani
siku ya mapumziko, watoto, mwenza wako wanakuhitaji, hata mifugo yako kama
ng’ombe na mbwa nayo inakuhitaji ndiyo maana siku ukitaka kuipa chakula huwa
inafurahi sana kwa sababu inahitaji uwepo wako.
Mpenzi msomaji kama umewahi kukumbana na
tatizo nililolieleza hapo juu, tafadhali tuma maoni yako na yatatoka wiki ijayo
kwenye kona hii. Pia usikose kutembelea ukurasa wetu wa Mimi na Uhusiano kwenye
Mtandao wa Facebook, Instagram na kundi la WhatsApp kujua mengi kuhusu mapenzi.
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.