Saturday, February 27, 2016

Published 2/27/2016 09:40:00 PM by with 0 comment

BAYO NA IMBORI-1

     
HALI ya hewa siku hiyo ilikuwa ya baridi sana kama ilivyozoeleka katika mji wa Manyara kiasi cha kufanya maeneo mengi kutulia tuli huku purukushani za kila siku zikiendelea kama kawaida.
Msichana Imbori alionekana mwenye majonzi mengi mbele ya baba yake mzazi Chifu Rohay Bariwe kwani siku hiyo ya Aprili 5, 1994  alitakiwa kufukuzwa mbele za watu  waliokuwepo nyumbani kwao hapo kwa kiongozi wao ili kushuhudia tukio hilo la kihistoria.

Miongoni mwa watu wote waliokuwepo  ni Isara, mke wa pili wa chifu Rohay Bariwe na mama mzazi wa Imbori na Marmo.
Kama ilivyokuwa kwa Imbori, Isara pia alikuwa mwingi wa huzuni, alilia sana akiwa  amemfumbata miguuni mwake mwanaye wa miaka sita aitwaye Marmo aliyekuwa akimshuhudia Imbori akifungashiwa mizigo michache ili kufukuzwa katika jamii hiyo ya Kabila la Wairaqw baada ya kukiuka miiko ya utamaduni.
Moyo ulikuwa unamuuma mno mwanamke Isara kwa sababu baada ya hapo hakukuwa na matumaini ya kumuona tena mwanaye mpendwa Imbori! Kama si kufa kwa kuliwa na wanyama wakali basi angeuawa na makabila ya watu walioishi msituni kwa kula nyama zikiwemo za binadamu.

“Kwa nini wasimsamehe tu!” msichana mmoja alisikika akimwambia jirani yake kwa masikitiko.
“Watajiletea matatizo kwenye familia yao.”
“Masikini Imbori!”
Watu wengi walionekana kugubikwa na majonzi kuliko kawaida, lakini ukweli ni kwamba hakukuwa na namna yoyote ya kulizuia jambo hilo! Imbori alifungashiwa mahindi ya kuchoma ndani ya furushi dogo, nyama-choma pamoja na karanga zilizobabuliwa kwenye moto. 

Akatakiwa kuondoka nje kabisa ya kijiji cha Luqandamuru kilichopo ndani ya Wilaya ya Mbulu mkoani Manyara.
“Mama na Marmo kwa herini, ninasikitika sitawaona tena...”
“Dada usiniachee  nakupenda sana...Dadaaa...” Marmo alichomoka mikononi mwa mama yake huku akipiga kelele za uchungu, akakimbia mpaka pale alipokuwa Imbori na kumkumbatia kwa nguvu hadi wakadondoka chini.
Kila mmoja alikuwa anafuta machozi! Ni ukweli kwamba walimpenda sana msichana huyo hasa kwa ustadi wake mkubwa wa kuimba nyimbo za majonzi kipindi cha kuwaaga mashujaa waliokuwa wanakwenda vitani kupambana na makabila yenye uadui na kabila lao.  Lakini hakukuwa na namna, kila aliyekwenda tofauti na utamaduni wao alitakiwa kutendewa hivyo.

“Kamtoeni huyo mtoto!” chifu Rohay Bariwe aliwaamuru walinzi wake kwa ujasiri huku akifuta machozi pia.
“Niacheni! Niacheni! Niacheee...” Marmo alijitahidi kufurukuta lakini alizidiwa nguvu, akarudishwa kule alikokuwa amekaa mama yake mzazi Isara.
   ***
Baada ya Marmo kuondolewa, Imbori aliinuka na furushi lake mkononi akaanza kupiga hatua za taratibu huku akisindikizwa na macho ya wanakijiji wenzake waliompenda mpaka pale alipotokomea kabisa kwenye upeo wa macho yao.
Nyuma yake aliacha minong’ono na vilio vingi! Wengi wa wasichana waliohudhuria katika tukio hilo walilaani juu ya mila na desturi za kabila lao wakisema, ziliwanyima haki ya msingi ya kuomba msamaha pale ambapo walikuwa wakidondokea kwenye makosa ambayo binadamu yeyote angeweza kufanya.
“Hizi mila haziwatendei haki wasichana wetu,” Qorro rafiki yake kipenzi na Imbori aliwaza huku machozi yakimmwagika.
***
Mwishowe saa nane zilikatika Imbori akivuka mabonde na milima, hatimaye majira ya saa 12 za jioni alikuwa ndani ya msitu wa Dakwii ulioaminika kutunza wanyama wakali wa porini lakini pia msitu huo ulikuwa unapakana na Kijiji cha Magara kwa upande wa kaskazini, kulikoishi jamii ya kabila la Wadatoga.
“Nakufa Imbori!” aliwaza msichana huyo huku akizidi kutembea, mashavuni kwake machozi yalikuwa yanabubujika kwa wingi.
Wakati huo giza lilikuwa limeanza kutanda katika anga la msitu huo, kwa mbali Imbori  alianza kuzisikia sauti za ndege na wanyama asiowaelewa.
Ghafla mapigo ya moyo wake yalianza kwenda mbio lakini hakuwa na jambo la kufanya zaidi ya kupiga moyo konde, akazidi kusonga mbele kwa ujasiri mkubwa, giza lilipozidi alitafuta mti uliomfaa akapanda ili ajisitiri kwa lengo la kuendelea na safari yake siku iliyofuata.
Akiwa juu ya mti huo, Imbori alijikuta akizama kwenye dimbwi zito la mawazo. Alikuwa anaiwaza familia yake, safari mpya ya maisha aliyokuwa ameianza.  Alimkumbuka pia mpenzi wake Bayo ambaye kwa wakati huo hakuwa anafahamu kuwa alikuwa hai au la!
                                     USIKOSE SEHEMU INAYOFUATIA
      edit

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.