Asanteni wasomaji wangu wote mlioguswa na mada ya wiki iliyopita. Ni kweli wengi imewaliza, imewakumbusha mbali lakini pia wengi imewafariji na kuwafanya waanze maisha mapya baada ya kuondokewa na wenza wao.
Kama nilivyoahidi wiki hii ni maalumu kwa maoni yenu juu ya mada hii hiyo ni kuwaonesha ni namna gani ninawapenda na kuwashirikisha katika magazeti yetu. Maoni ni mengi mno ila haya ni baadhi:
ALIFARIKI NIKIWA MJAMZITO
Pole na kazi kaka Gabriel, asante kwa maneno yako ya faraja, ni kweli kuondokewa na mtu uliyempenda inauma sana, haisahauliki. Mume wangu alinitoka Julai, mwaka jana nikiwa mjamzito wa miezi nane, kila nikimkumbuka naumia sana ila nimefarijika kwa mada yako.
NIMEFARIJIKA SANA
Nimefarijika sana na mada yako, inatufundisha na kutupa ari mpya ya kushukuru kwa kila jambo, kujituma, kuthubutu, kutokata tamaa na kadhalika, nakupongeza kwa ushauri wako mzuri na ninawashauri vijana tujifunze kupitia mada zako. Binafsi nasubiri sana kwa hamu sehemu ya pili ya mada hii.
Mimi Miss Annosiata
SITAPENDWA TENA
Mada hii imenigusa sana na imenifanya nishinde nalia kwani ni kama kuna mtu alikusimulia kuhusu maisha yangu ya mapenzi. Ni miezi mitatu iliyopita tangu mwenza wangu afariki dunia baada ya kugongwa na gari maeneo ya Kilimo-Kwanza mjini Dodoma, sitaki kuamini kama ni kweli kanitoka na sina uhakika kama nitampata mpenzi mwingine atakayenipenda kama yeye. Mungu ampumzishe kwa amani.
MUNGU AKUPUNGUZIE ADHABU YA KABURI
Nilikupenda sana baba watoto wangu, Khalid Abdallah ‘Baba Bitebo’ ila Mungu alikupenda zaidi, namuomba Mwenyezi Mungu akupunguzie adhabu ya kaburi, japokuwa tuliachana lakini bado moyo wangu unakukumbuka. Naamini Mungu atawaadhibu vibaka waliosababisha kifo chako kwa kukuchoma kisu. Mimi Shakira au Mama Anuary wa Msimbazi, Dar
PUMZIKA KWA AMANI MAMA
Mama yangu mpendwa, Neema Denis nakuombea kwa Mungu akupumzishe kwa amani, nitazidi kukupenda sana mpendwa mama yangu.
Mimi mwanao Nicolas Denis
XXLOVE IMENIJENGA
Pole kwa kazi ya kutuelimisha na kutupa tumaini jipya, mada yako ya ‘Mungu Aliyekupa, Amemchukua na Ndiye Atakupa Mwingine’ ilinigusa sana kwani nilifunga ndoa na nimpendaye ila baada ya mwaka mmoja kipenzi changu akanitoka, inauma sana, nilipoteza tumaini kabisa ila maneno yako yamenijenga, ubarikiwe.
NIMELIA SANA
Nilimpoteza mume wangu, Ismail ambaye alifariki dunia kwa kugongwa na basi. Kila ikifika Februari, 14 (Valentine’s Day) huwa namkumbuka sana. Niliposoma mada yako, nilijikuta nikibubujikwa na machozi mazito kwa saa kadhaa.
Valentine’s Day ilikuwa ni siku ya furaha kwangu na mpenzi wangu kama kuna kosa nilifanya alinirekebisha kwa upole huku akinibembeleza ila kwa sasa siku hiyo imegeuka machungu kwa kukumbuka kifo cha mpendwa wangu ambaye alikuwa tegemeo langu.
Naumia sana nikiwaona wenzangu wanatoka na waume zao, najikuta nashinda nikilia.
Mimi Farida Mohamed au Mrs Ismail
Mpenzi msomaji, usikose kutembelea ukurasa wetu wa Mimi na Uhusiano kwenye Mtandao wa Facebook, tu-follow Insta:@mimi_na _uhusiano au kujiunga kwenye group letu la WhatsApp kwa ushauri zaidi kuhusu mapenzi.
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.