Monday, February 8, 2016

Published 2/08/2016 06:51:00 AM by with 0 comment

KABLA YA KUANZISHA UHUSIANO MPYA, JIULIZE KWA NINI UMEACHWA?



Tumshukuru sana Mungu kwa kutujalia afya njema na kutukutanisha tena hapa kujadili na kupeana elimu ya uhusiano.

Wiki iliyopita tulijadili kuhusu kuachana na kuanza kuchukiana au kuwekeana visasi. Mada ya leo inahusu kukurupuka na kuanzisha uhusiano mpya baada ya kuachwa.Si jambo jema, unapaswa kujiuliza umeachwa kwa sababu gani? Ili hata kama ukiamua kuanzisha uhusiano mpya ujue ni mpenzi wa aina gani anakufaa?

Kabla hujaamua kuanzisha uhusiano mpya, unapaswa ujiulize kwanza maswali kadhaa kwa mfano; Nini kilichokufanya ukaachwa au kuachana na mpenzi wako? Je, uliachwa kwa sababu wewe ni maskini au siyo wa hadhi yake? Au huna elimu ya kutosha kama alivyo yeye? Au anahisi kwa elimu yako hapaswi kuwa na mpenzi mwenye umaskini wa elimu, fedha au upeo kama wewe?

Je, umeachwa kwa sababu wewe hujishughulishi (mvivu) unapokuwa faragha kwenye kupeana mashamsham au kukaa kwako kama gogo ndiko kumemkimbiza mpenzi wako? Au pengine umeachwa kwa sababu tu siyo msafi wa mwili na mpenzi wako ana hulka ya usafi? Au unatoa harufu kwa sababu kuna watu wanatoa harufu mbaya mdomoni, kwapani na kwingineko? Kama hujawahi kubaini hilo kama ni tatizo basi jaribu kulichunguza nalo.

Au umeachwa tu kwa sababu ya tabia ya mpenzi wako ya ukiruka njia na ujana mwingi?
Jiulize pengine mpenzi wako ameshinikizwa na ndugu au rafiki zake kwa sababu ya tabia zako f’lani na wanajitahidi kumuepusha ndugu yao.

Au kwa sababu wewe ni bahili au huna mtazamo wa maisha endelevu ya baadaye zaidi ya kuwaza tu kula bata.
Au kwa sababu ya matumizi yako kuwa makubwa kuliko kipato cha mpenzi wako, jiulize mwenyewe au unapenda sana kuombaomba mshiko na unachokifanya hakionekani.
Kama utajiuliza maswali hayo na mengine mengi kabla ya kuanzisha uhusiano, nina uhakika utapata jibu zuri sana litakalokuwa sehemu ya muongozo mzuri katika uhusiano wako mpya kwa sababu utakuwa umeshajua wewe ni mtu wa aina gani.
 

Pia utakuwa umeshajua ni mpenzi wa aina ipi anayekufaa, atakayekuvumilia kasoro zako, ingawa mapenzi hayatabiriki sana ila ni vizuri kujua kasoro na sifa za mpenzi anayekufaa.

Kila mwanadamu ana upungufu wake ila kwa kuzingatia niliyoyaandika hapo juu utapunguza kuumia na kuumizwa kwa sababu ya kuachwaachwa hovyo, tena kwa vijisababu vya ajabu visivyokuwa na kichwa wala miguu.
Makala haya yanawazungumzia wapenzi wa jinsi zote kwa maana ya mwanamke na mwanaume kwani baadhi ya tabia zinashabihiana.

Angalizo; mapenzi hayahitaji uchaguzi wa elimu, kipato, rangi, ufahari, kabila, dini na kadhalika. Kuna watu wana elimu ya kutosha, wameolewa na walala hoi kwa sababu ya kupata penzi tamu na analolihitaji. Kuna watanashati na warembo wameolewa na watu wa kawaida sana kiasi cha kila mtu kushangaa mtaani wakiwaona wawili hao, wengine utasikia wakisema ‘hata hawaendani kabisa’.

Mfano mwingine kuna baadhi ya mastaa wa fani mbalimbali huamua kuwa na uhusiano au kuoa mtu asiye na umaarufu wowote ili kuufurahisha moyo wake.
Xxlove-GPL
      edit

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.