Monday, February 29, 2016

Published 2/29/2016 06:11:00 AM by with 0 comment

WALIMU KUPANDA DALADALA BURE DAR



MANENO YA DC PAUL  MAKONDA; Kwa ufupi ni kwamba, wazo hili limejengwa juu ya msingi wa sababu kubwa tatu. Moja, kwa kuzingatia changamoto za nauli za mara kwa mara wanazolazimika kuzilipa walimu ili kuyafikia kwa wakati maeneo yao ya kufanyia kazi na pili, ni kuhakikisha mimi na serikali yangu ya wilaya ya Kinondoni tunakuwa sehemu ya juhudi za Mheshimiwa Raisi za kuboresha maslahi na mazingira ya walimu ya kufanyia kazi ili matarajio ya ndoto yake anayoipigania usiku na mchana ya kutaka kuiona sekta ya elimu nchini ikikua kwa kasi yanatimia.



Na tatu, ni kuwafanya walimu wa wilaya ya Kinondoni na Dar es Salaam kwa ujumla kama watumishi wenzangu wa serikali nao wanafaidi sehemu ya matunda ya serikali yao ambayo kwa dhati imedhamiria kubadilisha maisha yao ili na wao waweze kubadilisha maisha ya vijana wetu kupitia taaluma.
Kwasababu hizo nilizozianisha hapo juu ninaomba kuwatangazia walimu wangu wa shule zote za serikali kuanzia za msingi mpaka sekondari ya kwamba, sasa watasafiri bure wanapokwenda kutufundishia wadogo zetu na watoto wao. 


Hii ni baada ya kufanya vikao na mazungumzo ya kina na wamiliki wa vyombo vya usafiri wa umma kupitia vyama vyao vya Darcoboa na Uwadar na hatimaye mazungumzo hayo kuitimishwa na mkutano wa vyama vyote hivyo viwili vya wamiliki wa vyombo vya usafiri ambao kwa sauti moja wamekubali kuniunga mkono kwenye utekelezaji wa wazo langu hili.
Kipekee na kwa unyenyekevu mkubwa, naomba kuchukua fursa hii kuwashukuru sana wamiliki hawa wa vyombo vya usafiri wa umma pamoja na viongozi wa vyama vya Darcoboa na Uwadar kwani walikuwa na kila sababu ya kukataa hasa ukizingatia kuwa wao ni wafanyabiashara na tena wanazo changamoto nyingi katika sekta yao ya usafirishaji, wengine wakiwa hata wamekopa kwenye mabenki ili wapate uwezo wa kufanya biashara, lakini kwenye jambo hili wote kwa umoja wao wameseme ndio na wako tayari kuanza haraka iwezekanavyo.

Utaratibu kwa walimu juu ya utumiaji wa fursa ambayo tumeipata utakuwa kama ifuatavyo:- Moja, nimemuelekeza ofisa elimu wa sekondari na shule za msingi, kutoa maelekezo kwa wakuu wa shule zote za serikali zilizopo wilayani kwangu na wilaya nyinginezo za jiji la Dar es Salaam, kutengeneza vitambulisho vya shule zao vitakavyokuwa na picha ya mwalimu, jina lake kamili, jina la shule anayofundisha, namba ya simu ya mkuu wa shule husika pamoja na saini yangu mimi mwenyewe Paul Makonda ili kuepuka udanganyifu.
Nimewataka zoezi hili walifanye na kulikamilisha ndani ya wiki moja ambapo baada tu ya kukamilika itakuwa ni furaha yangu kuwatangazia walimu wote wa shule za serikali jijini Dar es Salaam kuwa, watakuwa wakipanda daladala bure ila tu kwa siku za jumatatu mpaka Ijumaa na kwa muda wa saa kumi na moja asubuhi mpaka saa mbili asubuhi na kati ya saa tisa mpaka saa kumi na mbili jioni. Ingawa, kila mwalimu atalazimika kuonyesha kitambulisho chake alichotengenezewa kwenye shule yake pamoja na kile cha ajira ya serikali.


      edit

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.