MPENZI msomaji wa Love & Life napenda
kukukaribisha katika mada nzuri ya wiki hii inayosema siku mojamoja, kila mpenzi
ashinde na simu ya mwenzake…tuone!
Nianze kwa kusema tu, naamini mada hii itakuwa
ni ngumu sana kwa wapenzi wa zama hizi za kizazi kipya, bila kujali wahusika kama
ni wapenzi, wachumba au wanandoa, bado ugumu nauona akilini mwao.
Kwa nini?
Kama kweli mnapendana hakuna ugumu wowote,
ila ugumu unakujaje? Ninaamini kama utamuachia mpenzi wako simu yako, kwa tabia
zako za kutokuwa mwaminifu, ni hakika atakutana na madudu mengi sana na hapo
ndipo ugumu wa kumwachia mwenza wako simu yako unapoanzia.
Simu ni chanzo kweli?
Kama ulikuwa hujui tambua sasa kwamba, katika
ulimwengu huu wa utandawazi, simu imekuwa ndiyo chanzo kikubwa cha kusababisha kuvunjika
kwa ‘mahusiano’ miongoni mwa wapendanao.
Hii yote inachangiwa na kuwepo kwa mitandao
mbalimbali ya kijamii kwa nia ya kurahisisha mawasiliano.
Tatizo kwenye mitandao kila mtu mzuri
Kwa mitandao mingi, iwe WhatssAp, Twitter, Facebook,
Badoo, Instagram na mingine mingi, kila mtu anajitahidi kuweka picha nzuri
itakayomuonesha yeye akiwa mrembo (kama ni mwanamke) au mtanashati (kama ni
mwanaume). Hii yote ni kwa ajili ya kuwavutia michepuko.
Sasa utakuta mtu tayari yupo kwenye uhusiano
lakini akavutiwa na mwingine wa kwenye Facebook, basi wanaunga hapohapo na
usaliti unaanza.
Kila mtu na simu yake
Ni jambo la kawaida kwa wapenzi, wachumba au
wanandoa kila mtu kuwa bize na simu yake kwa muda wote na kila mtu hayuko
tayari kuona mwenzake kashika simu yake. Ndiyo maana walio wengi unakuta
wameweka namba za siri (password) ili hata kama mwenza wake ataishika basi
asiweze kuzama ndani na kutazama chochote bila idhini yake, hasa michepuko ya
kwenye mitandao.
Miujiza itokee
Natamani siku moja, kila mmoja katika wawili
walio kwenye uhusiano ashinde na simu ya mwenzake. Watakaofanikiwa na siku
ikapita salama bila kukumbana na vimeo au michepuko ya aina yoyote ile, naamini
uhusiano wao utachipuka upya na kuaminiana na penzi lao litadumu.
Angalizo
Kama hizi simu tusipoziangalia na kuzitumia
vizuri kwa ajili ya kudumisha uaminifu na kujenga uhusiano ulio bora, basi
kizazi hiki kitavunja rekodi kwa wawili walio kwenye uhusiano wa kimapenzi kutokuwa
waaminifu na uenda uhusiano wao kuvunjika.
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.