Na.M&U
Ilipoishia….
Wakati zikiwa zimebaki dakika kumi na tano kabla ya ndege
hiyo kuruka tena, Mbelike anastukia simu yake maalumu ya kijasusi ikiita kwenye
saa yake ya mkononi. Alipoiangalia anashangaa ikiwa inatoka ikulu ya Tanzania.
Endelea
nayo…
Haraka haraka aliingia chooni na kuanza kuongea na mtu wa
upande wa pili, ambaye alimpa maagizo ya kurudi Tanzania haraka iwezekanavyo,
kwani kuna kazi ambayo alitakiwa kuja kuifanya.
Kwa kutambua umuhimu wa hicho alichoitiwa, Mbelike hakuwa
na jinsi zaidi ya kufuata amri ya mkuu wake wa kazi, bwana Innocent Kembo, mkuu
wa shirika la kijasusi nchini, TISS.
Mara moja alifanya utaratibu wa kupata ndege iliyokuwa
ikirudi Tanzania. Bahati nzuri aliipata ambayo ilikuwa ikiondoka nusu saa
baadaye. Muda wa ndege hiyo kuondoka ulipofika, Mbelike na abiria wengine
walikuwa tayari kwenye viti vyao huku wakiwa wamefunga mikanda yao baada ya
kupata maelekezo kutoka kwa wahudumu wa ndege hiyo.
Baada ya saa kadhaa angani, hatimaye waliwasili kwenye
uwanja wa ndege wa kimataifa wa mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Alipokelewa
na watu wa usalama na kisha kuingia kwenye gari mojawapo kati ya mbili za
ikulu, na safari ya kuelekea ikulu ilianza.
Njiani alikuwa na mawazo mengi juu ya wito uliokatisha
safari yake ya kikazi nchini Marekani. Alijuwa kutakuwa na jambo zito mno kwani
haikuwahi kutokea oparesheni zikaingiliana katika kazi zake.
Magari yalizidi kuchanja mbuga huku wakipita njia za mkato
kukwepa foleni za jiji hilo. Hatimaye baada ya dakika kadhaa, walifika na moja
kwa moja walinzi waliokuwa zamu walifungua geti kuruhusu gari hizo kuingia
ndani.
Aliteremka na kwenda kuonana na mkuu wake ofisini kwake.
Lakini alishangaa kutomkuta, na sekunde chache baadaye alifika mtu na
kumuelekeza aelekee kwenye chumba cha siri cha mikutano cha ikulu.
Aliongoza hadi chumbani humo na kumkuta bwana Kembo akiwa
na watu wengine watano ambao hakuwatambua pamoja na mheshimiwa rais. Hakushtuka
sana kuwaona watu hao ndani ya chumba hicho ambacho ni nadra sana kutumika, ila
hofu iliyomwingia ni juu ya wito wa ghafla kiasi hicho.
Je ni
wito gani huo uliofanya akaghairishiwa safari yake ya kikazi nchini Marekani?
Tukutane
kesho, muda kama huu.
Kwa USHAURI, MIKASA YA KWELI YA MAPENZI, HADITHI, MACHOMBEZO, USHUHUDA NA UJASIRIAMALI Jiunge na M&U WhatsApp kwa Na 0657486745 kwa MADA ZA KILA SIKU. Pia tembelea https://www.facebook.com/mimi-na-uhusiano-1584071311866497/… au https://www.instagram.com/mimi_na_uhusiano au www.miminauhusiano.blogspoti.com
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.