- SEHEMU YA 9
- Mpenzi msomaji, wiki iliyopita niliishia pale kama ambavyo Zakayo na Haruni walivyokuwa hawaamini kama kweli sharobaro Nelly angeweza kufanya kazi ya ujenzi, Dorren naye kushangazwa na jambo hilo ambapo moyoni alisema:
- “Huyu kijana piga ua garagaza siyo fundi, nahisi atakuwa kaja kumpeleleza baba yangu, sijawahi kumuona sharabaro tena anayevaa miwani na mwenye dimponsi anafanya kazi za ujenzi.”
- Wakati Doreen anawaza hayo, fundi Yassin na Nelly walibadilisha nguo na kuvaa za kufanyia kazi kisha fundi huyo alimwambia Zakayo amwelekeze Nelly kazi ya kufanya.
- Baada ya Zakayo kuambiwa hivyo na kumuona Nelly akiwa kabadili nguo na kuvaa za kazi ambazo hata hivyo hazikuwa chakavu kama walizokuwa wakifanyia yeye na Haruni, kidogo aliamini kwamba Nelly pia alikuwa pale kikazi.
- Kufuatia fundi kumwambia amwelekeze Nelly kazi ya kufanya, hakutaka siku hiyo ya kwanza kumpa kazi ngumu akamwelekeza ya kuzoa mchanga uliokuwa pembeni ya nyumba kubwa waliyoishi akina Doreen.
- “Kaka wakati sisi tunaendelea na kazi ya kuweka malumalu ndani, wewe zoa huu mchanga na kuusogeza pale kwani kesho tunataraji kuanza kuweka malumalu hapa pote,” Zakayo alimwambia Nelly.
- Kwa kuwa eneo ambalo ulikuwepo mchanga ambao Nelly aliambiwa hauzoe lilikuwa karibu na chumba alichokuwa akilala Doreen, msichana huyo mrembo alisikia maongezi yao.
- Baada ya Zakayo kumwelekeza Nelly kazi ya kufanya akaingia nyumba kubwa walikokuwa wakiweka malimalu na kumkuta fundi Yassin akimwelekeza kazi ya kufanya Haruni.
- “Vipi umemwelekeza?” fundi Yassin alimwuliza Zakayo.
- “Tayari bro ila mpaka dakika hii siamini kama huyo kijana anaweza kufanya kazi hii ngumu tunayofanya, yule amekaa kimayaiyai,” Zakayo alimwambia fundi Yassin, wakacheka.
- “Kwa kuwa kapigika kimaisha, kwa hiyari yake kanifuata na kuniambia anataka kuja kunisaidia kazi ili aweze kupata fedha, si unaelewa maisha ni fedha?” fundi Yassin aliwaambia.
- “Ni kweli bro lakini kwa huyo kijana akimaliza siku tatu hapa nitajua kweli amedhamirilia,” Haruni alichagiza, wakacheka.
- Wakati fundi Yassin akizungumza na wasaidizi wake hao wa kazi kazi, kule nje Nelly alianza kuchota mchanga kwa kutumia chepe na kuurushia eneo aliloelekezwa na Zakayo bila kujua Doreen alikuwa akimchungulia kupitia dirishani.
- “Yaani siamini, huyu kaka na uhandsome wake wote huu na miwani juu anafanya kazi hii, lazima kaja hapa kumpeleleza baba yangu tu maana watu wa usalama wa taifa ni balaa,” Doreen aliwaza.
- Wakati mrembo huyo anawaza hivyo, Nelly aliyechota mchanga kama chepe ishirini hivi alipozi na kujinyoosha mgongo kutokana na ugumu wa kazi aliyokuwa akifanya.
- “Huyu siyo fundi mbona anaonekana kuchoka haraka,” Doreen aliyekuwa bado anamchungulia Nelly pale dirishani aliwaza.
- Baada ya kupita kama dakika arobaini hivi tangu aanze kazi, Nelly alihisi kiu akaingia ndani walikokuwa wakifanya kazi fundi Yassin na akina Zakayo.
- “Vipi Nelly, unaendeleaje? Hii kazi yetu haina udogo lakini utazoea kadiri siku zinavyokwenda,” fundi Yassin alimwambia.
- “Sawa bro, ila nimebanwa na kiu sijui nitapata wapi maji ya kunywa?” Nelly alimwambia fundi Yassin.
- Kwa kuwa mafundi hao walipokuwa wanahitaji maji ya kunywa waliwasaliana na Anne msichana wa kazi wa akina Doreen, Haruni alitoka na Nelly, akaanza kumwita Anne.
- Licha ya kumuita mara kadhaa, Anne hakuitika ndipo Doreen alifungua dirisha na kumfahamisha kwamba Anne alikuwa ametoka kidogo.
- “Poa dada, huyu fundi mgeni anahitaji maji ya kunywa,” Haruni alimwambia Doreen.
- Baada ya kuambiwa hivyo, Doreen alimwambia sawa na kumtaka Nelly apite mlango wa uani kisha aingie jikoni.
- Kwa kuwa Nelly hakufahamu mlango huo, alimuomba Zakayo ambaye alikuwa mwenyeji amuoneshe ndipo fundi huyo akamuonesha.
- Nelly alizunguka nyuma ya nyumba hiyo na kuuona mlango wa kuingia jikoni alipotembea hatua kama mbili hivi mlango ulifunguliwa na Doreen, macho yao yalipogongana, kila mmoja akaachia tabasamu bila kujua sababu za kufanya hivyo.
- “Samahani unataka maji ya baridi au ya moto?” Doreen alimwuliza Nelly ambaye tayari akili yake ilihama baada ya kuona shepu nzuri ya Doreen.
- “Kwa hiki kijoto yabaridi yatakuwa mazuri,” Nelly alimwambia Doreen.
- “Karibu usubiri ndani wakati nakuandalia,” Doreen alimwambia Nelly.
- “Hapana sista wewe niletee tu hapa nje,” Nelly aliyekosa kujiamini alimwambia Doreen.
- “Jamani wewe kaka ingia ndani unaogopa nini?” Doreen ambaye alikuwa akilindwa sana na wazazi wake asitoke nyumbani kuhofia wanaume wakware alimwambia Nelly.
- Usikose kuhudhuria Semina ya Mimi na Uhusiano (M&U). Mada Kuu: “KUNA MAISHA NJE YA MAUMIVU YA MAPENZI.” Itakayofanyika Agosti, 27 mwaka huu kwenye Ukumbi wa Malaika Hall, Kijitonyama. kwa maelezo zaidi wasiliana nasi kwa namba 0657486745 au tembelea ukurasa wetu wa Mimi na Uhusiano kwenye Mtandao wa Facebook au tembelea www.miminauhusiano.blogspot.com
- Usikose kesho muda kama huu…
Tuesday, August 16, 2016
Published 8/16/2016 11:52:00 AM by Mimi na Uhusiano 'M&U' with 0 comment
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.