Ni wazi kwamba hakuna wito wowote duniani ambao hauna changamoto, kumbe basi kila wito ambao umeuchangua kuuishi tarajia kukutana na changamoto na wala usijidanganye kuwa wito Fulani ndiyo bora kwani hakuna familia iliyokuwa salama kwa kila kitu. Baada ya wanandoa kufunga ndoa huwa wanakua na maisha ya furaha na amani siku za mwanzo ila kadiri siku zinavyokwenda kila mmoja anaanza kupoteza thamani ya mwenzake taratibu.
Pale mtu anapoamua kufunga ndoa kwa hiyari yake yeye mwenye anakuwa na shauku na hamasa ya kumfurahia mwenzake kuishi naye pamoja na kutambua thamani ya mwenzake.
Baada ya wanandoa kutarajia kupata kitu Fulani kutoka kwa mwenza wake na kukosa kile alichotarajia kukipata basi anaanza kupoteza ladha au thamani kwa mwenza wake. Mwanzo kila mmoja anakuwa kama chumvi yenye ladha katika chakula lakini baadaye mmoja wa wanandoa anaweza kuwa chumvi iliyokosa thamani katika mahusiano yao.
Kama tunavyojua rafiki, kazi ya chumvi ni kuleta ladha katika chakula je kama wewe uko katika mahusiano ya ndoa na mwenzako ukishamuona kama chumvi iliyokosa thamani, yaani iliyopoteza ladha huwezi kumfurahia hili tunaweza kuliona hata katika mfano wa chakula kilichokosa chumvi huwa hakina ladha kabisa na unakuwa huna hamasa ya kukila chakula hicho.
Kila mmoja huenda amepoteza ladha kwa mwenzake pengine kwa kushindwa kumtimizia mwenzake haja yake au njaa yake. Kama tunavyojua wanandoa ambao ni mwanamke na mwanaume wote hawa kila mmoja ana njaa yake hivyo ukishindwa kushibisha njaa ya mwenzako unakuwa umepoteza ladha au thamani hivyo unakuwa kama chumvi iliyopoteza ladha.
Mwanamke na mwanaume ni viumbe viwili ambavyo kila mmoja anatoka katika sayari yake. Wanaume wanatokea katika sayari ya mars na wanawake nao wanatokea katika sayari ya venas. Kutokea katika sayari tofauti maana yake hawafanani na wako tofauti,
Mbinu itakayoweza kurudisha thamani katika mahusiano yako ni mbinu ya negative visualization yaani taswira hasi. Hii ni mbinu ya wanafalsafa wa ustoa yaani stoic philosophy iliyotumiwa na wanafalsafa wa zamani kama vile zeno, Seneca kabla hata ya Yesu kuzaliwa kuishi maisha bora yenye furaha na mafanikio makubwa .
Rafiki, kujenga taswira hasi kwa mwenzi wako wa ndoa itakusaidia kurudisha ladha au upendo uliopotea kwa mfano kama unahisi mwenzi wako amepoteza thamani kwako anza kumjengea taswira hasi jenga picha akili kabisa tayari ameshakufa kwa sababu kila ulichonacho hapo sasa umepewa kwa muda tu utaviacha tu. Kama umevuta taswira hasi mwenzi uliyekuwa naye ndiyo hayupo tena na hapo mwanzo alikuwa na thamani kubwa basi ndiyo utaanza kuona thamani yake.
Jenga taswira hasi kuwa mwezi uliye naye sasa hivi kesho siyo wako utanyang’anywa kwa hiyo, kama ulikuwa haumpi thamani utaanza kumthamini huku ukijua kuwa utanyang’anywa muda wote wote kwa hiyo, lazima utampa thamani ya hali juu sana. Hata asubuhi unavyomuaga mwezi wako jenga taswira kuwa kama ndiyo mara yako ya mwisho kuonana naye kwa hiyo unatakiwa kumwaga kwa thamani na kumtumia vizuri kwa muda huo ambao upo naye. Wazungu wanasema never take any things for granted yaani usichukulie kitu chochote kama kipo tu au umepewa kirahisi, kama una mke , mume wako mtumie vizuri sasa kipindi yuko hai hata siku akifa hutojutia kuliko kumchukulia yupo tu kila siku na huoni thamani yake.
Unaweza kuitumia mbinu hii katika mahusiano yoyote yale uliyonayo kama una mama yako yuko hai basi mtumie vizuri kabla hajaondoka kwani kila uliye naye sasa hivi umeazimwa kwa muda. Ni sheria ya asili kuwa hakuna mtu atakayeishi milele, na hakuna mtu ambaye ana mkataba wa kudumu wa kuishi milele na yule aliye naye sasa. Kama uko katika ndoa basi kila mmoja anatakiwa kujiandaa kisaikolojia kuwa yeye ni mjane mtarajiwa. Kama unamuaga rafiki yako basi muage vizuri` na kuamini kuwa hiyo ndiyo siku yako ya mwisho kuonana naye.
K ama umejenga taswira hasi kwa mwenzi wako hutoweza kumchukulia kirahisi hata kama ana mapungufu kiasi gani lazima utatumia vizuri uwepo wake. Ishi na mwenzi wako huku kila mmoja akimtumia mwenzake vizuri na kutumia thamani yake vema huku akiamini kuwa muda huo ambao mko sasa ndiyo muda wenu wa mwisho kuwa pamoja. Kama unambusu na kumkumbatia mtoto wako, mwenzi wako basi mbusu kwa thamani kubwa huku ukiamini kuwa ndiyo mara yako ya mwisho kumfanyia vitu hivyo.
Lazima kujitoa kwa moyo na kutambua thamani ya mwenzako kama ukimjenga taswira hasi ya kuwa uko naye hapo kwa muda tu hivyo unatakiwa kumtumia vizuri kabla hajaondoka.
Hatua ya kuchukua, tumia mbinu hii ya negative visualization yaani taswira hasi kurudisha amani, upendo, furaha , thamani katika maisha yako ya ndoa na mahusiano yako na watu wengine. usimchukulie huyo uliye naye sasa hivi yupo tu kimazoea bali mchukulie wa thamani kubwa kwamba unanyang’anywa muda wote wote ule ni sawa sawa na ukiambiwa kuwa umeme utakatika baada ya dakika chache na utarudi baada ya wiki mbili hakika kama una nguo za kunyoosha lazima utanyoosha haraka tena za wiki nzima hutoweza kuuchukulia tena upo kwani tayari umeshaambiwa hautokuwepo tena hivyo lazima utautumia vizuri kabisa.
Mwisho, kila mtu ana udhaifu wake na thamani yake hivyo tumia vizuri thamani yake kwa kipindi ambacho uko naye sasa ili hata akiondoka hutoweza kujutia kwa sababu ulimtumia vizuri. Chochote unachomfanyia mwenzi wako jenga taswira hasi kuwa ndiyo siku ya mwisho kumfanyia kitu au jambo hilo hivyo huwezi kufanya kimakosa utahakikisha unajitoa kwa moyo wote. Usitafute ubaya kwa mwenzako kwani ukitafuta ubaya tarajia tu kuupata.