Watu wengi wamekuwa hawavipi kipaumbele kikubwa vipaji vyao, huwa wanaona ni kama kitu ambacho kipo na hivyo hakuna anayeweza kukilipia. Lakini tumekuwa tunaona watu wachache wakinufaika na vipaji vyao. Watu kama wasanii, wachezaji na wanamuziki wamekuwa wanatumia vizuri vipaji ambavyo vipo ndani yao.
Je unawezaje na wewe kutumia vipaji vilivyopo ndani yako na kuvifanya kuwa biashara ambayo itakutengenezea kipato kikubwa?
Kwanza kabisa, kabla hata hatujaangalia jinsi ya kugeuza kipaji chako kuwa biashara, tukubaliane kitu kimoja, inawezekana kugeuza kipaji chochote kuwa biashara. Siyo tu kwenye sanaa na michezo, bali kitu chochote kile, ambacho kinaweza kuongeza thamani kwa wengine kwa kuwatatulia matatizo au kuwaletea furaha kinafaa kugeuzwa kuwa biashara. Iwe ni uandishi, uzungumzaji, uongozi, upangaji na mengine mengi, kuna namna unaweza kutumia kibiashara.
Yafuatayo ni mambo muhimu katika kugeuza kipaji chako kuwa biashara;
1. Jua kipaji au vipaji vyako ni nini.
Kwanza kabisa ni lazima ujue kipaji au vipaji vilivyopo ndani yako, hili ni zoezi ambalo unahitaji kulifanya wewe mwenyewe. Wewe unajijua kuliko mtu mwingine yeyote, hivyo angalia maisha yako tangu unakua mpaka sasa na angalia ni vitu gani unapenda sana kufuatilia au kufanya. Ukijitathmini kwa umakini utagundua kuna baadhi ya vitu unapendelea kuliko vitu vingine. Hapa usijihukumu kama unachopendelea ni kizuri au kinakubalika na wengine, unachohitaji ni kutambua kile kinachokusukuma, kinachoweza kukuamsha asubuhi ukiwa na hamasa na uhakika wa kwenda kufanya mabadiliko kwenye siku yako.
2. Jua thamani unayoweza kuongeza kwa wengine kupitia kipaji au vipaji vyako.
Biashara ni thamani, unalipwa kulingana na thamani unayotoa kwa wengine. Kadiri unavyotoa thamani kubwa ndivyo unavyopata mapato makubwa na ukitoa thamani ndogo utalipwa kidogo pia. Ukishajua vipaji vyako unachohitaji kujua ni thamani ipi unaweza kuitoa kwa wengine. Na hili pia ni zoezi rahisi kufanya kama utajitathmini maisha yako yote. Angalia ni vitu gani au maeneo gani ambayo watu wamekuwa wanakutegemea sana kwenye kipaji ulichonacho. Ukishayajua maeneo haya na kuona ni vitu gani ambavyo watu wanahitaji sana, unaweza kuboresha zaidi kile unachowapatia na kuanza kutoza gharama. Kama unachotoa ni bora, utapata watu wengi walio tayari kulipia.
Kwa mfano kama wewe unapenda sana kufuatilia mchezo fulani, na watu wakawa wanakuja kwako ili kusikia maoni yako kuhusu mchezo huo, tayari wewe una thamani ambayo wengine wanaihitaji. Unaweza kukusanya taarifa za kutosha kuhusu mchezo huo na kuziweka kwenye mfumo ambao unaweza kuwauzia wengine. Kipaji chochote, hata kama ni upishi, kuna namna nyingi ambazo unaweza kuzitumia na kuongeza thamani kubwa kwa wengine.
3. Usiogope kutoza gharama.
Tatizo kubwa sana kwenye kugeuza kipaji kuwa biashara huwa linaanzia hapa, watu wanaogopa sana kuwatoza watu wengine fedha. Wanaona kama wataonekana ni watu ambao wanajali zaidi fedha kuliko kuwasaidia wengine. Hii inakuwa hivyo kwa sababu hapo awali wengi walishazoea kupata kile unachotoa bure kabisa. Iwe ni kwa ushauri au msaada mwingine wowote, wengi wataanza kukujua kwa kuwa unafanya bure. Usikubali kupotezwa na hili, hakikisha unaandaa kitu chenye thamani bora na usiogope kuwatoza watu gharama. Kama kuna watakaokuambia kwa nini uweke gharama basi jua hao siyo muhimu na hawajali sana kwa kile unachotoa.
Hakuna dhambi kwenye kuwatoza watu gharama kama unawapatia thamani ambayo inafanya maisha yao kuwa bora zaidi. Unachohitaji kusimamia wewe ni thamani bora na inayowafanya watu kuwa na maisha bora.
Kama kila mmoja wetu angeweza kutumia kipaji chake kuwa sehemu kuu ya kipato chake, tungekuwa na jamii zenye furaha na watu wenye mafanikio. Hii ni kwa sababu biashara bora ni ile ambayo mtu anaipenda kutoaka moyoni, biashara hii inapotokana na kipato, mtu anaipenda sana. Hata kama tayari una biashara nyingine, hata kama kwa sasa umeajiriwa, fikiria vipaji vyako ni nini na anza kutoa thamani kwa wengine. Unaweza kuanza bure kwa mwanzoni ili watu wajue una nini, na baadaye ukaanza kuwatoza watu fedha kulingana na thamani unayotoa.
Kwa Ushauri Wa Mahusiano, Mada Za Mahaba, Hadithi, Machombezo, Mikasa Ya Kweli Ya Mapenzi Na Ujasiriamali. Jiunge na M&U SMS au M&U WhatsApp kupitia Na. 0679979785.
Pia tembelea www.miminauhusiano.blogspot.com, Insta:@mimi_na_uhusiano au tembelea ukurasa wetu wa Mimi na Uhusiano kwa ku-Bonyeza Hapa
Na.M&U